Psalms 65

Kusifu Na Kushukuru

(Kwa Mwimbishaji: Zaburi Ya Daudi. Wimbo)


1 aEe Mungu, sifa zakungojea katika Sayuni;
kwako wewe nadhiri zetu zitatimizwa.

2 bEwe usikiaye maombi,
kwako wewe watu wote watakuja.

3 cTulipokuwa tumefunikwa kabisa na dhambi,
wewe ulisamehe makosa yetu.

4 dHeri wale uliowachagua
na kuwaleta karibu ili waishi katika nyua zako!
Tunashibishwa kwa mema ya nyumba yako,
mema ya Hekalu lako takatifu.


5 eUnatujibu kwa matendo ya kushangaza ya haki,
Ee Mungu Mwokozi wetu,
tumaini la miisho yote ya duniani
na la bahari zilizo mbali sana,

6 fuliyeumba milima kwa uwezo wako,
ukiwa umejivika nguvu,

7 guliyenyamazisha dhoruba za bahari,
ngurumo za mawimbi yake,
na ghasia za mataifa.

8 hWale wanaoishi mbali sana
wanaogopa maajabu yako,
kule asubuhi ipambazukiapo
na kule jioni inakofifilia
umeziita nyimbo za furaha.


9 iWaitunza nchi na kuinyeshea,
waitajirisha kwa wingi.
Vijito vya Mungu vimejaa maji
ili kuwapa watu nafaka,
kwa maana wewe umeviamuru.

10 jUmeilowesha mifereji yake
na kusawazisha kingo zake;
umeilainisha kwa manyunyu
na kuibariki mimea yake.

11 kUmeuvika mwaka taji ya baraka,
magari yako yanafurika kwa wingi.

12 lMbuga za majani za jangwani umezineemesha;
vilima vimevikwa furaha.

13 mPenye nyanda za malisho pamejaa makundi ya wanyama,
na mabonde yamepambwa kwa mavuno;
vyote vinashangilia kwa furaha na kuimba.
Copyright information for SwhKC